Ndizi ni chakula kikuu kwa wengi na ni zao la uhakika wa chakula, lakini huathiriwa sana na mnyauko bakteria wa migomba.
Ugonjwa huu ni hatari sana na unaweza kuangamiza shamba lote la migomba ndani ya muda mfupi kama hautadhibitiwa. Ugonjwa huo huenezwa kwa njia njia 2 kuu; kupitia zana za ukataji zilizo na maambukizi kama vile panga na majembe, na ndiyo njia kuu ya uenezaji katika maeneo ambayo wakulima hutumia sana zana za shambani. Njia ya pili ya maambukizi ni kupitia wanyama na wadudu kama vile ng‘ombe, kondoo, nyuki na vidukari. Hii ni kawaida ambapo wakulima hawatumii sana zana za shambani.
Ishara na dalili
Migomba iliyoambukizwa inaweza kuchukua muda wa kati ya siku 14 hadi 90 kabla ya kuonyesha dalili zozote za ugonjwa. Kipindi hiki kinaitwa maambukizi ya kisiri na ni kipindi cha hatari zaidi na chanzo cha maambukizi. Wakulima hueneza ugonjwa katika kipindi hiki bila kujua.
Mara nyingi ugonjwa huu hujidhihirisha na kukauka kwa majani kabla ya kukomaa, kuchomwa kwa majani, kuiva mapema kwa matunda kabla hayajakomaa, na kuoza kwa mashina ya migomba.
Udhibiti wa ugonjwa
Udhibiti unaofaa zaidi ni kudumisha usafi katika mashamba yote ya migomba, kuondoa machipukizi yote ya kiume kwenye mimea kwa kutumia kifaa maalum, kuua viini kwa vifaa vya shamba vinavyotumiwa kwenye mimea iliyo na ugonjwa, na matumizi ya mbegu safi za migomba kutoka vyanzo vinavyoaminika.
Iwapo wakulima wanashuku maambukizi ya mnyauko bakteria, ni lazima wasitishe shughuli zote za shamba ambazo ni pamoja na kupogoa, kulima na kuvuna majani Baada ya miezi 3, mkulima anaweza kujua ni migomba gani imeathiriwa na kwa kiwango gani.