Lengo la wakulima ni kupata mavuno mazuri mwishoni mwa msimu. Kuna hatua ambazo zinafuatwa ili kupata mavuno bora.
Kuandika tarehe ya kupanda ni muhimu kwa sababu kila aina ina kipindi chake cha kukomaa. Hii humsaidia mkulima kuhesabu ni lini mazao yatakuwa tayari kuvunwa. Katika maharagwe ya soya, aina fulani hukua mapema na huchukua kati ya siku 85 hadi 95 kukomaa, huku nyingine zikichelewa kukomaa na huchukua siku 115 au 125. Mbaazi kwa ujumla ni zao linalokomaa mapema na hufikia ukomavu kati ya siku 65 hadi 70. Fanya maandalizi muhimu ya kuvuna wakati wa kuvuna unapokaribia.
Dalili za ukomavu
Soya na mbaazi vinapokomaa, majani hugeuka manjano na kudondoka. Maganda ya mbegu hubadilika kutoka kijani kibichi hadi manjano wakati mimea inakaribia kukomaa. Maganda pia hubadilika kutoka manjano hadi kijivu au kahawia kutegemea aina .
Maganda yaliyokomaa yanapaswa kuonekana makavu, na unaweza pia kuchukua sampuli ya mbegu ili kuona kama mbegu zako ziko tayari kuvunwa. Kwa soya, rangi ya mbegu hubadilika kutoka kijani kibichi hadi manjano hafifu wakati kwa mbaazi, mabadiliko ya rangi hutegemea aina.
Kuvuna nafaka
Ili kuwa na nafaka bora, vuna wakati viashiria vya ukomavu vinapokuwa dhahiri. Uvunaji wa aina zilizopasuka maganda haupaswi kucheleweshwa.
Uvunaji unaweza kufanywa kwa kutumia kisu kikali kwa kukata mimea kwenye usawa wa udongo au kung’olewa na kuwekwa kwenye turubai.