Malisho ni nyenzo muhimu sana katika ufugaji wa kuku na ni kigezo kikuu cha mafanikio ya ufugaji wa kuku.
Iwapo una ujuzi kidogo au huna ujuzi wowote kuhusu utengenezaji wa chakula cha kuku, unaweza kutengeneza chakula chenye sumu au chakula cha ubora duni. Hatika hali hii, kuku wa mayai hawatataga kwa wakati sahihi au watataga mayai machache, wakati kuku wa nyama hawatafikia uzito wa soko baada ya wiki 6.
Vijenzi vya malisho ya kuku
Unapotengeneza malisho, vitu vikuu zinazohitajika ni mahindi kwa ajili ya nishati, wishwa wa ngano au mahindi kwa ajili ya fumuele, na soya ambayo hutoa protini. Mbadala pekee ya soya ni ufuta, lakini unashauriwa kutumiwa na watu wa kitaalamu tu kwa sababu una kiwango kikubwa cha mafuta, na hivyo huongeza kiwango cha mafuta kwenye malisho. Malisho haya yakipewa kuku wa mayai, huongeza mafuta mwilini mwa kuku, na hivyo hatataga mayai.
Unapotumia soya kama chanzo cha protini, ikaange au ipike, kwa sababu soya mbichi ina sumu.
Unaweza kutumia mabaki wa alizeti au mabaki ya mbegu za pamba. Iwapo utatumia mabaki ya mbegu za pamba, hakikisha kwamba hazijapakwa dawa, kwa sababu dawa inaweza kusababisha sumu.
Unaweza pia kuongeza dagaa ingawa hazipendekezwi kwa kuku wa mayai kutokana harufu kali ambayo inaweza kupitishwa hadi kwenye mayai. Pia hupunguza muda wa kuhifadhi mayai kwa sababu ya protini nyingi iliyomu.
Mwisho unahitaji chokaa. Ikiwa malisho ni ya kuku wa mayai, unahitaji asilimia 3% ya chokaa, kwa kuku wanaokua unahitaji asilimia 1.5%, na kwa vifaranga unahitaji asilimia 1.3%. Chokaa ni muhimu sana kwa kuku wa mayai.