Mavuno ya mahindi yanaweza kupunguka sana ikiwa magugu, wadudu na magonjwa hayatadhibitiwa.
Baadhi ya wadudu waharibifu wa mahindi ni pamoja na vipekecha shina, dumuzi, vifukuzi, panzi, nzige, mchwa, vidukari, nondo, utiriri, viwavi, viwavijeshi, nakadhalika.
Udhibiti wa wadudu waharibifu wa mahindi
Ili kudhibiti wadudu, hakikisha zao la mahindi lina afya bora ili kuweza kupambana na wadudu.
Panda mapema ili kuepuka idadi kubwa ya wadudu wanaotokea ukichelewa kupanda. Kagua viwango vya wadudu walio shambani, na uwadhibiti wanapoanza kusababisha uharibifu. Tunza wadudu marafiki wa wakulima ambao husaidia katika udhibiti wa kibiolojia.
Tumia viuatilifu, huku ukibadilisha aina zavyo ili kupunguza uwezekano wa wadudu kupata upinzani dhidi ya kemikali.
Fanya mzunguko wa mazao, lakini epuka kupanda mazao yanaoshambuliwa sana na wadudu katika mpango wa mzunguko. Panda mmea mitego ili kudhibiti wadudu. Panda aina sugu dhidi ya wadudu.
Udhibiti wa magonjwa ya mahindi
Utambuzi wa ugonjwa ni muhimu sana katika udhibiti. Magonjwa ya kawaida ni pamoja na mnyauko, uozo, ukungu, bakajani, kutu, na fugwe ya suke.
Ili kudhibiti magonjwa, kagua shamba mara kwa mara, badilisha mazao, tumia mbegu safi zilizothibitishwa, hakikisha shamba la mahindi ni safi na halina magugu.
Udhibiti wa magugu
Magugu hupunguza mavuno kwa kushindania maji na virutubisho. Zingatia usimamizi wa magugu kabla ya kupanda mahindi. Dhibiti magugu kwa kutumia mbinu jumuishi za usimamizi ambazo ni pamoja na kulisha magugu kwa mifugo, kutumia mbegu zisizo na magugu, kupanda mbegu ambazo huota vizuri, kupalilia kwa wakati sahihi.