Misitu ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia ambayo husaidia katika suala la kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Misitu ni njia ya pili ya kuondoa kaboni hewani baada ya bahari, na huondoa takribani asilimia 19% ya kaboni inayozalishawa ulimwenguni kote. Misitu na udongo hufanya kama njia za kuondoa kaboni kwa sababu huhifadhi kaboni dioksidi (hewa ukaa) wakati wa mchakato wa usanidimwanga.
Umuhimu wa misitu
Misitu hutenda jukumu muhimu katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa njia kadhaa yaani; huondoa, huhifadhi na hubadilisha kaboni.
Katika uondoaji wa kaboni, miti hunasa kaboni dioksidi (hewa ukaa) kutoka kwenye angahewa na kuihifadhi kama kaboni kwenye majani hai na baadaye kwenye majani yaliyokufa, pamaoja na udongo.
Katika uhifadhi, bidhaa za mbao zinazotokana na misitu huhifadhi kaboni. Bidhaa hizi pia zinaweza kutumika kama mbadala wa nyenzo zisizoweza kurejeshwa ambazo pia hutoa gesijoto hatari zaidi.
Kupanda miti
Usimamizi endelevu wa misitu unaweza kukabiliana na athari za gesijoto kupitia upandaji miti kwa madhumuni ya kupanua eneo la misitu. Kupanda miti mingi hutoa mbao zenye ubora wa juu zaidi kwa ajili ya ujenzi, kutengeneza fanicha, pamoja na kuzalisha nishati.
Lengo ni kufupisha mzunguko wa uzalishaji, kwani miti michanga ina ufanisi zaidi katika kunyonya hewa ukaa (kaboni dioksidi) kuliko miti mizee.
Uchaguzi wa aina za miti zilizopandwa unahitaji kurekebishwa na kusahihishwa ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Ni muhimu kupunguza ukataji miti ovyo, na kurejesha misitu iliyoharibiwa katika hali yao ya awali