Kahawa ni chanzo kikuu cha mapato kwa wakulima lakini huathiriwa na magonjwa.
Magonjwa makuu ya kahawa ni pamoja na chule buni (CBD), kutu ya majani (CLR) na bakajani (BBC). Dalili kuu za CBD ni pamoja na madoa ya hudhurungi kwenye maua, mabaka madogo meusi kwenye matunda, rangi ya hudhurungi kwenye shina la miti na vidonda vya kahawia vilivyo na madoa madogo meusi. Udhibiti wa CBD ni pamoja na kupogoa, kupunguza matawi makuu, kunyunyizia viuatilifu vinavyofaa, kupanda aina sugu na kubadilisha aina zinazoweza kushambuliwa, pamoja na kukata sehemu za juu za mibuni ili kuhimiza ustahmilifu.
Magonjwa mengine
Dalili za kutu ya majani (CLR)ni pamoja na madoa ya unga wa manjano ambayo huonekana upande wa chini. majani yote yanaweza kuambukizwa, kukauka na kudondoka iwapo maambukizi ni makali. Usimamizi wa kutu ya majani ni sawa na ule wa chule buni.
Bakajani ni ugonjwa mwingine hatari wa kahawa. Dalili zake ni pamoja na vidonda vyeusi na pembezoni zilizolowekwa na maji ambayo huonekana kwenye majani mwanzo wa mvua. Majani yaliyokufa na yaliyokauka hayadondoki lakini hubakia kwenye mmea na maambukizo hushambulia machipukizi ya matawi, na kisha huenea chini. Wakati ugonjwa unaendelea, mti mzima unaweza kuonekana mweusi. Maua hubadilika meusi na mmea mzima hufa. Udhibiti ni kwa kupanda miche yenye afya, kukata sehemu zilizoambukizwa, kupanda miti ya kivuli na kunyunyiza dawa za ukungu. Pogoa miti yote mara baada ya kuvuna ili kupunguza matukio ya magonjwa.
Mnyauko; Hii husababisha kunyauka na mmea mzima hufa. Hudhibitiwa kwa kupunguza tindikali ya udongo, kuondoa wadudu, kung‘oa na kuchoma miti iliyoambukizwa.
Kuunganisha au kubebesha mkahawa
Hii husaidia kubadilisha aina zinazoshambuliwa na magonjwa kuwa sugu kwa kuunganisha. Kikonya huchaguliwa kutoka kwa mche wa miti mama. Kubebesha huokoa gharama ya kung‘oa mikahawa yote na kupanda upya.