Coir ni nyuzi za maganda ya nazi zilizokomaa. Wakati wa usindikaji, tunapata bidhaa ya taka inayoitwa coir pith, ambayo huozeshwa na kutumika kama mbolea.
Mbolea hii ni muhimu sana katika maeneo ya ukame ambapo hasa kuna udongo wa kichanga, ili kuboresha uhifadhi maji ya udongo. Kwa kiasili, coir pith hupatikana kwa kuloweka maganda ya nazi ndani ya maji kwa wiki kadhaa. Kisha, maganda ya nazi huondolewa ndani ya maji na kupondwa kwa kijiti cha mbao. Baadhi ya wakulima huendesha trekta juu ya maganda ya nazi yaliyolowekwa, huku wengine wakitumia mashine. Kisha nyuzi hizo hutumika kutengeneza kamba, mikeka nakadhalika, huku pumba za nazi zikibadilishwa kuwa mboji.
Mchakato wa kutengeneza mbolea
Taka za maganda ya nazi huchujwa na kuwekwa kwenye eneo lililo na kivuli au mti ili kuoza. Rundo la mbolea hutengenezwa katika safu; tandaza safu ya kwanza ya takriban kilo 20 za nyenzo, na ongeza kiozaji kilicho na vijidudu vingi.
Kiozaji kinaweza kutengenezwa kwa kuchanganya lita 100 za maji na kilo 5 za samadi ya ng‘ombe, ndizi 10 zilizopondwa, lita 3 za mkojo wa ng‘ombe, nusu kilo ya sukari guru, nusu kilo ya unga, na kiganja kimoja cha udongo. Changanya haya na uyakoroge mara mbili kwa siku, kisha uyafunika na gunia. Baada ya wiki moja, hii itakuwa tayari kutumika.
Nyunyiza lita 10 za kiozaji kwenye safu ya pumba za nazi, kisha ongeza takribani kilo 4 za nyenzo iliyo na nitrojeni, kwa mfano samadi ya kuku.
Ongeza safu ya pumba za nazi, na kisha rudia mchakato. Gramu 100 za mbegu za uyoga au 100g trichodema zinaweza kutumika kama viozaji. Nyunyiza maji kwenye rundo kila siku ili kutunza unyevu. Fungua mbolea kila baada ya siku 10 ili kuingiza hewa safi. Mbolea itakuwa tayari baada ya mwezi mmoja.
Kutumia mbolea
Weka 100kg ya mbolea hii mwishoni mwa utayarishaji wa shamba. Kwa vitalu, changanya sehemu 1 ya mbolea na sehemu 4 za udongo kabla ya kujaza viriba au trei za mbegu.
Kwa miti ya matunda hadi miaka 10, weka 10kg kwa mmea kila baada ya miezi 6, na kwa miti ya matunda zaidi ya miaka 10, weka 15kg kwa mmea kila baada ya miezi 6.