Kuweka matandazo ni hatua muhimu katika usimamizi wa miti na mazao. Hat hivyo, kuna makosa ya kawaida ambayo wakulima hufanya katika mchakato huo.
Kosa la kwanza ni kwamba wakulima huweka matandazo karibu sana na msingi wa shina la mmea. Kuweka matandazo karibu sana na shina la mmea haishauriwi kwa sababu miti ya matunda haioti mizizi kwenye eneo la shina, kwa hivyo matandazo yote yanapaswa kuwekwa umbali fulani kutoka kwenye shina la mti kwa sababu hapo ndipo mizizi hukua.
Uozo wa shina la mti
Kuweka matandazo karibu na shina la mti husababisha uozo wa shina, ugonjwa ambao hauna tiba. Ugonjwa huo hujidhihirisha kwa kudondosha majani, pia majani huanza kugeuka manjano kama vile upungufu wa nitrojeni, na mti huanza kunyauka kutoka juu hadi chini au kutoka chini kwenda juu kulingana na ukali wa hali hiyo.
Hili linaweza kuzuiwa kwa kusogeza matandazo inchi moja au 2 kutoka kwenye shina la mti ili kuhakikisha kuwa hakuna unyevu unaokusanywa kuzunguka msingi wa shina la mti.
Makosa mengine
Kosa lingine ambalo wakulima hufanya ni kuweka matandazo juu sana hadi urefu wa inchi 5 hadi 6 kutoka ardhini. Hii huongeza uwezekano wa shina la mti kuoza kwa sababu matandazo huteleza hadi kwenye shina la mti hata ukijaribu kuyaondoa.
Matandazo yanapaswa kuwa inchi 3 juu ya ardhi kwani huku kunasaidia kuhifadhi unyevu kwenye udongo, husaidia kuhifadhi joto kwenye udongo, huruhusu mti kuwa na kipindi cha kukauka cha kutosha, jambo ambalo huzuia uozo wa shina la mti.
Aina ya matandazo yanayotumika ni kosa lingine linalofanywa na wakulima. Hii ni kwa sababu matandazo yaliyotengenezwa kwa plastiki yana rangi, na mara yanapooza rangi na nyenzo nyingine za matandiko haya huingia kwenye mti na udongo, jambo ambalo kusababisha madhara hasa kwenye udongo badili ya kuulinda.