Ufuta ni rahisi kukuza, lakini mbinu duni za kuvuna, kupura na kuhifadhi zinaweza kupunguza ubora wake. Mawe, changarawe na taka nyingine zinaweza kuchanganyika na mbegu za ufuta na hivyo kuathiri bei.
Ufuta ukikomaa sana shambani, maganda hupasuka na kuachilia mbegu. Ufuta huwa tayari kuvunwa wakati mabua au mashina yanakuwa manjano, majani huanza kudondoka na vifuko vya chini hubadilika kahawia.
Kushughulikia ufuta
Siku chache kabla ya kuvuna, andaa eneo la kukaushia sakafuni au katika kiwanja kilichokaribu. Lazima eneo hilo liwe safi, kavu na lilindwe dhidi ya wadudu na wanyama waharibifu. Eneo la kukaushia linaweza kutengenezwa kwa kuchanganya kinyesi cha ng‘ombe, udongo laini, chumvi na maji. Samadi ya ngombe na udongo hufanya ardhi kuwa ngumu, chumvi huzuia chungu na mchwa kushambulia ufuta. Mabunda ya ufuta pia yanaweza kukaushwa juu ya paa za nyumba ili kuzuia wanyama wasiharibu mbegu.
Kuvuna ufuta
Kabla ya kuvuna, nuwa ringa au kisu cha kuvunia ili kurahisisha uvunaji. Wakati wa kuvuna, kata mabua ya ufuta 10cm juu ya ardhi lakini usitikise mabua kwa sababu mbegu zitadondoka chini. Baada ya kuvuna, acha mabunda shambani kwa masaa kadhaa.
Kusanya mabunda na uyapeleke katika eneo la kukaushia. Fanya mabunda kwa kusimamisha wima mimea uliyokatwa huku vifuko vya mbegu vikiangalia juu.
Kupura na kusafisha mbegu
Pura ufuta wako angalau siku 15 baada ya kukausha kwenye turubai au damani ya plastiki. Huku kunafanywa kwa kutikisa mashina ya ufuta kwa mikono au kutumia kijiti.
Chuja mbegu kupitia vichujio viwili tofauti ili kuondoa mawe, takataka ya mimea na vumbi, na baada ya hapo pepete mbegu na uziweke kwenye magunia safi yaliyoshonwa vizuri.
Hifadhi mbegu kwenye eneo safi lisilopenyeza mvua, na lina hewa ya kutosha. Weka magunia ya ufuta juu ya mbao au magogo ambapo hawagusi ardhi moja kwa moja ili kulinda ufuta dhidi na unyevu.