Shamba nzuri la pilipili huanza kwa miche thabiti yenye afya. Hii inaweza kufanyika kwa kuandaa kitalu kizuri, kuandaa shamba vizuri na kushughulikia miche wakati wa kupandikiza.
Ili kukuza miche ya pilipili yenye ubora mzuri katika kitalu, unafaa kurutubisha na kulainisha udongo, na kumwagilia maji ya kutosha. Andaa kitalu kiwe cha upana wa mita 1, na karibu na shamba ili iwe rahisi kupandikiza miche. Panda mbegu chache tu kwa kila mtaro.
Kanuni au miongoza ya kupandikiza
Andaa shamba mapema kwa kuondoa magugu na kulainisha udongo. Kisha ongeza mboji au mbolea, kwani pilipili hukua vyema kwenye udongo laini, uliyo na rutuba.
Pandikiza wakati miche ina nguvu ya kutosha kujisimamisha yenyewe, lakini usiiache ikae kwenye kitalu kwa muda mrefu. Kuacha nafasi kati ya mimea hutegemea tabia ya ukuaji wa pilipili. Aina inayomea wima inafaa kupandwa kwa mwachano wa 40cm kwa 40cm, na mwachano wa 40cm kwa 80cm kwa aina inayotambaa.
Pandikiza miche jioni. Mwagilia maji kitalu kabla ya kupandikiza ili iwe rahisi kuondoa miche bila kuiharibu.
Unapopanda, punguza mizizi ya miche ikiwa ndefu sana ili mimea istawi vizuri. Panda mche mmoja katika kila shimo kwa kina cha takribani 5cm. Hakikisha kwamba unapandikiza kwa uangalifu.
Baada ya kupandikiza, miche hunyauka kidogo, na hii ni kawaida. Mwagilia miche maji ili iweze kustawi.