Nzi wa matunda hutaga mayai yao kwenye matunda na mboga. Tunaweza kudhibiti nzi wa matunda kwa kukusanya na kuharibu matunda yaliyoanguka.
Nzi wa matunda hushambulia na kutoboa aina nyingi ya matunda na mboga nyingi ili kutaga mayai yao. Matunda yaliyoshambuliwa na nzi huanguka mapema. Ukifunga tunda lililoshambuliwa, mabuu ya nzi wa matunda (funza) huonekana. Usipokusanya matunda haya, mabuu hutoka ndani ya matunda na kuingia kwenye udongo.
Baada ya wiki 1, mabuu huacha matunda na kuhamia kwenye udongo ambapo hubadilika kuwa kifukofuko cha kahawia. Wiki moja baadaye, nzi wa matunda huanguliwa kutoka kwenye kila kifukofuko.
Kuharibu matunda yaliyoanguka.
Nzi wengi wanaweza kutoka kwenye tunda moja lililoanguka. Kwa hivyo, ni muhimu kuondoa na kuharibu matunda yote yaliyoanguka angalau mara moja kila wiki.
Mbali na maembe na machungwa, nzi pia huathiri aina nyingine za matunda kama vile parachichi na korosho. Kwa hivyo yakusanye matunda haya pia na kuyaharibu. Mabibo ya korosho hukomaa haraka kuliko maembe na yanaweza kubeba nzi wa matunda. Kwa hivyo, vuna mabibo yakikomaa na pia yakusanye na kuchoma yote yaliyoanguka.
Unaweza kuharibu matunda yaliyokusanywa kwa kuyazika kwenye shimo lenye urefu wa mita 1, na ukanyage udongo uliyojuu ili mabuu yasipenyeze. Unaweza pia kuweka matunda yaliyoanguka kwenye mapipa na kuyafunika vizuri, au kwenye mifuko myeusi ya plastiki isiyo na mashimo. Funga mifuko baada ya kuweka matunda. Weka mifuko juani kwa wiki moja au mbili ili kuua mayai na wadudu. Unaweza kutumia mabaki ya matunda kama mbolea shambani.