Mbegu nyingi za mpunga huharibiwa zikipandwa kwa kutawanya. Ili kupunguza uharibifu huo, unafaa kutengeneza kitalu cha mbegu wiki mbili kabla ya kuatika au kuhamisha miche.
Wakulima mara nyingi hupanda kwa kutawanya kabla ya msimu wa mvua. Lakini mvua inapochelewa, mbegu zilizo katika udongo huharibika, na wakulima wanafaa kupanda upya tena.
Kuatika/ kuhamisha miche
Kuatika kuna manufaa, kwani kunaokoa mbegu, maji na virutubisho. Kwa kuatika, una uwezo wa kukuza miche bora. Kuatika hutunza mimea dhidi ya magugu na hata kurahisisha usimamizi wake, kama vile kupalilia.
Kutengeneza kitalu cha mbegu
Miche haifai kuwa na majani zaidi ya manne wakati yanapandikizwa au kuatikwa. Tengeneza kitalu ili kiwe karibu na maji, shamba, na katika mwangaza wa jua. Ni muhimu pia kuzingatia usalama wa kitalu chako kutokana na uharibifu wa wanyama. Na pia, kuwa hakina mchanga mwingi, kwa sababu hukauka haraka. Katika maeneo ya mabonde, maji ya mvua hutiririka chini ya mteremko. Kwa hivyo unafaa kutengeneza upande mrefu wa kitalu uwe wima kwa mteremko.
Tengeneza kitalu kiwe cha upana wa mita 1 na urefu wa mita 10. Ukubwa huo ni rahisi kufanyika kazi nao. Tayarisha na kusawazisha kitalu, ili maji ya mvua yasichukuwe mbegu zote yakitiririka. Vunjavunja udongo hadi uwe laini na uongeze mbolea, ili mbegu ziweze kuchipuka kwa urahisi na mizizi iwe na nguvu. Limbikiza udongo wa kitalu uwe juu zaidi ya 10 cm, ili kuzuia uharibifu wa mbegu kutokana na maji. Katika maeneo ya umwagiliaji, sawazisha kitalu, ili kuwezesha kumwagilia vizuri.
Kwa kitalu ambacho kina urefu wa mita 10, unahitaji kilo mbili za mbegu. Kiwango hiki kinaweza kutumika kwa upanzi wa shamba la mita za mraba 500. Fanya mbegu ziote Kabla ya kuzipanda, hivyo weka mbegu katika gunia na uziloweshe maji kwa muda wa siku 1. Kisha ondoa mbegu kutoka kwa maji na uziweke mahali panapopitisha hewa kwa siku moja hadi mbili mpaka zianze kuota.
Funika mbegu na udongo kidogo. Ongeza samadi kidogo ya ngombe ili kuboresha udongo na kudhibiti ndege. Tandaza majani makavu juu ya kinga la kivuli ili kuzihifadhi mbegu ziwe unyevu, na kuzilinda dhidi ya ndege. Ondoa majani haya baada ya siku 3 hadi 4. Tumia matawi kujenga kinga la kivuli lenye urefu wa takribani mita 1.5 juu ya kitalu. Tunza kinga la kivuli kwa kutumia majani ya mitende na kumwagilia maji mara kwa mara. Katika muda wa wiki moja, kitalu hiki kitakuwa na nguvu na unaweza kuondoa kinga la kivuli.