Kwa kuwa ni zao linalohitajika sana kutokana na umuhimu wake, ukuzaji na uzalishaji wa kahawa huathiriwa na mambo mbalimbali ambayo ni pamoja na bungua mweusi wa mashina ya mikahawa na rutuba duni ya udongo.
Bungua mweusi ni mdudu mdogo mweusi unaong‘aa ambao una urefu wa 1–2 mm, na umbo la mviringo. Mdudu huo hukaa kwenye matawi ya mikahawa. Bungua jike hujipenyeza kwenye tawi na kuchimba mashimo ya ukubwa wa pini.
Kutambua wadudu
Uwepo wa wadudu hutambuliwa kwa urahisi na dalili kama vile majani kugeuka njano, mashimo madogo chini ya matawi, vumbi nyeupe kwa mashimo ya kuingilia, na matawi dhaifu.
Dalili zingine ni kunyauka, majani na matawi kubadilika rangi kuwa meusi kutoka kwenye shimo la kuingilia na kuelekea juu ya tawi lililoathirika.
Udhibiti wa wadudu
Kuna haja la ukaguzi wa shamba wa kila siku ambao husaidia katika kutambua wadudu, na hivyo kuwadhibiti mapema. Ondoa sehemu za mmea zilizoathiriwa na uzichome ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa.
Ongeza mbolea shambani ili kustawisha mimea, mwagilia maji na punguza kivuli shambani.
Epuka kupanda miti ambayo huhimiza bungua mweusi wa mashina ya mikahawa.