Kwa kuwa ni biashara yenye faida kubwa, ubora na wingi wa bidhaa zinazopatikana kwa ufugaji wa kuku aina ya fayoumi hubainishwa na mbinu ya uzalishaji inayotumika.
Kuku aina ya foyoumi hufugwa kwa madhumuni ya kutoa mayai kibiashara, na ni sugu dhidi ya magonjwa kuliko kuku wengine, na pia wana wateja wengi. Kuku hawa huanza kutaga mayai wakiwa na umri wa miezi 6, na hutaga wastani wa mayai 182–280 kila mwaka.
Usimamizi wa kuku aina ya fayoumi
Kwanza, ufugaji wa kuku aina ya fayoumi ni biashara yenye faida kubwa ikiwa utunzaji sahihi utatekelezwa. Kuku hawa ni sugu, na hustahimili magonjwa. Mwanzoni, nunua vifaranga vya ubora wa juu vyenye afya, na visivyo na magonjwa. Unaweza kununua vifaranga vya siku moja au kuku waliokomaa.
Jenga banda bora ili kulinda ndege dhidi ya wanyama wawindaji, hali mbaya ya hewa, na pia kudumisha afya ya kuku. Tumia nyenzo zinazopatikana kama vile mianzi au zilizotengenezwa kwa saruji ili kujenga banda.
Mfumo wa kufugia ndege ndani hupendekezwa katika ufugaji wa kuku aina ya fayoumi. Katika hili, acha nafasi ya futi 4–5 za mraba kwa kila ndege, na ujenge banda kwa njia ambayo inaruhusu usafishaji kwa urahisi. Kulisha ndege ni jambo muhimu sana katika biashara ya ufugaji wa kuku. Kwa hivyo, wape chakula bora ili kuwawezesha kukua vyema na kuwa na afya njema. Pia lisha kuku vyakula vya maduka vilivyotengenezwa tayari, au vyakula vilivyotengenezwa na wewe mwenyewe.
Kuku aina ya fayoumi hula majani wanaporuhusiwa kutembea huru. Kamwe usimpe kuku vyakula vilivyochafuliwa, na kila mara uwape maji safi ya kutosha. Kuku aina ya fayoumi huzaliana vizuri wanapofugwa katika uwiano mzuri wa dume 1 kwa majike 10.
Hatimaye, kwa vile kuku aina wa fayoumi hustahimili hali ya kiangazi na magonjwa, wanahitaji utunzaji kidogo. Tunza kuku ipaswavyo kwa kuwafuatilia na kuwachanja mara kwa mara.