Mbolea ya minyoo inaweza kutengenezwa shambani kwa kuandaa kitalu cha mbolea. Katika utengenezaji wa kitalu cha mbolea, ni vyema uwe na aina mbalimbali za vyanzo vya kaboni kwa sababu viumbe hai vidogo hupenda kula nyenzo zozote za kikaboni.
Kutengeneza mbolea ya minyoo
Ili kutengeneza mbolea ya minyoo, vyanzo vya kaboni utakavyotumia vinaweza kuwa majani makavu, taka ya jikoni na majani ambayo tayari yameoza. Majani yaliyooza ni chanzo kizuri cha vijidudu naviumbe hai mbalimbali ambavyo husaidia kuvunjavunja chakula kabla hakijaliwa na minyoo.
Vipande vidogo vya mbao vinaweza pia kuongezwa na kufanya kama chanzo cha muda mrefu cha kaboni kwa minyoo kwani vinachukua muda mrefu kuoza kikamilifu .
Iwapo unatumia nyasi kama chanzo cha kaboni, kuwa mwangalifu kuhakikisha kwamba nyasi unayotumia haikunyunyiziwa dawa za kuua magugu.
Loweka vyanzo vya kaboni katika madini kama chumvi ili kuvirutubisha. Hii pia ni muhimu katika kuongeza virutubisho kwenye mbolea ya minyoo.
Weka mchanganyiko wa nyezo hizo za kikaboni kwenye mfuko wa kutengenezea mbolea na pia ongeza minyoo. Minyoo humeng’enya nyenzo na kuzalisha mbolea ya minyoo. Baada ya miezi 4 hadi 5, nyenzo zitakuwa zimeoza. Unaweza kuvuna mbolea ya minyoo na kuongeza nyenzo nyingine kwenye mfuko.
Hakikisha kuwa hakuna unyevu mwingi kwenye mfuko wa kutengenezea mbolea.
Katika mfuko wa mbolea, usiweke bidhaa za maziwa, nyama, vitunguu wala vitunguu saum. Hizi ni bora kuwekwa kwenye shimo la mbolea.