Makazi ya mbuzi pamoja na aina ya mbuzi ni mambo muhimu katika biashara ya ufugaji wa mbuzi.
Unapofuga mbuzi kibiashara, jenga banda la mbuzi. Banda linaweza kujengwa chini au kuinuliwa. Hata hivyo, hakikisha kuwa unatunza usafi katika banda kwa sababu uchafu husababisha vifo vya wanambuzi.
Banda la mbuzi lililoinuliwa
Unapojenga banda la mbuzi, hakikisha kuwa limeinuliwa hadi urefu unaopendekezwa yaani angalau mita 1 kwenda juu ili kuruhusu mtu kuingia chini na kulisafisha. Umuhimu wa kuinua banda ni kutenganisha wanyama na kinyesi.
Banda la mbuzi linapaswa kujengwe pembezoni mwa uzio na sio katikati. Hii hurahisisha usimamizi bora, yaani mbuzi huingia bandani kwa urahisi kwa sababu wanyama hupenda kingo/pembe.
Kuondoa mbuzi wasiofaa
Kufuga mbuzi wasiozaa huleta hasara shambani mwako, kwa sababu unagharamia kuwalisha na kuwasimamia, kwa hivyo ni bora kuwaondoa.
Pia, ondoa mbuzi wazee. Mbuzi wazee huwa na nywele zinadondoka kutoka kwenye ngozi na pua zao. Kitaalamu, umri wa mbuzi unaweza kujulikana kwa kuangalia meno yake. Anapokua kikamilifu, mbuzi atakuwa na jozi 4 za meno. Meno huanza kulegea akiwa na miaka 7, akiwa na miaka 8 huanza kuwa mafupi na akiwa na miaka 10, meno huanza kutoka.
Mbuzi wazee wana kingamwili duni na ikiwa wana ugonjwa, uwezekano wa kupona ni mdogo. Pia mbuzi wazee huzaa mara moja au kutozaa kabisa kwa mwaka, wakati mbuzi wanatakiwa kuzaa mara mbili kwa mwaka.