Ulimwenguni kote, watu hutumia ndizi kwa njia mbalimbali kama vile kupika, kuchoma na kupanda. Maganda ya ndizi pamoja na migomba hukatwakatwa na kulishwa mifugo.
Hata hivyo, migomba na ndizi zina adui mkubwa anayeitwa fukusi wa migomba. Fukusi wa migomba ni mdudu mdogo mweusi aliye na mdomo mrefu uliyojikunja. Mimea iliyoshambuliwa na fukusi wa migomba hukua polepole na kutoa matunda madogo.
Maisha ya fukusi wa migomba
Fukusi jike hutaga mayai yao chini ya shina la mgomba juu ya ardhi au kwenye shina lililokatwa na kuachwa baada ya kuvuna.
Mayai huanguliwa kuwa mabuu ambao hutoboa shimo kwenye shina la mgomba. Mashimo hayo huzuia mpito wa maji na virutubisho kuelekea kwenye shina, na hivyo kudumaza ukuaji wa mgomba. Kadri mabuu wanakua, ndivyo mashimo kwenye mashina yanavyopanuka na mwishowe huelekea ardhini. Mashimo hayo hudhoofisha mashina na kuyafanya yavunjike sehemu ya chini au katikati.
Kutambua fukusi wa migomba
Migomba iliyoshambuliwa huzaa mikungu midogo, magamba ya majani hupasuka. Kutakuwa na mashimo kwenye shina na matunguu, na hivyo huvunjika.
Fukusi wa migomba huenda umbali mfupi na ni nadra sana kuruka. Fukusi wa migomba huenea kwenye mashamba mpya kupitia vipanda vilivyoathiriwa. Hakikishwa unatumia vipanda safi ili kuzuia kueneza fukusi.
Kudhibiti fukusi wa migomba
Baada ya kupanda migomba, dumisha rutuba ya udongo na unyevu wa kutosha shambani mwako ili kupata mimea yenye afya, na inayoweza kustahimili wadudu na magonjwa.
Ongeza mbolea shambani kwa umbali wa 2ft kutoka kwenye shina la mgomba ili mizizi isimee karibu sana juu ya ardhi. Tandaza shamba ili kuhifadhi unyevu wa udongo ili kuzuia fukusi kushambulia shina la mgomba.
Mashina yaililokatwa hivi majuzi huvutia fukusi sana, kwa hivyo kila baada ya mavuno kata mashina katika vipande vidogo vidogo na uvitandaze ili vikauke haraka. Mashina yaliyovunwa yanaweza kutumiwa kama mitego ya fukusi. Wachome fukusi waliwoshikwa.