Maembe hutoa manufaa kadhaa za kiafya. Hata hivyo, maembe huharibika haraka, ni mazito kusafirisha, pamoja na wakulima hupata bei duni katika msimu wa mavuno. Wakulima wanaweza kupunguza hasara kwa kukausha maemba kuwa achari ambazo ni tamu, na zinauzwa kwa bei nzuri.
Kikaushiaji cha jua hutumiwa kukausha maembe kwa sababu hakina gharama, na ni cha bei nafuu kwa wakulima wengi. Kupata achari nzuri, anza na kuchagua maembe mazuri. Maembe yanafaa kuwa yamekomaa vyema, hayana kasoro, wala hayajatobolewa na nzi weupe. Pia yanafaa kuwa yameiva ili upate achari bora. Safisha mikono kwa maji safi na sabuni kabla ya kuanza kushughulikia maembe. Pima na kuchagua maembe kulingana na ubora ili kupata achari bora. Safisha maembe vizuri kabla ya kuambua, na pia safisha trei ili kuepuka uchafuzi.
Kukaushia kwa jua
Unapoambua, anza kwa kukata upande wa shina kisha uambue kuelekea mwisho. Tumia kisu kikali au kifaa kinachochongea maembe ili kupata achari laini na kupunguza uwezekano wa kujikata. Kata vipande virefu vilivyonyooka ukihakikisha kwamba vipande vyote vinalingana. Baada ya kutandaza vipande vya maembe katika trei, viweke kwenye kikaushiaji cha jua ili vyote vikauke kwa haraka na usawa. Kisha funga mlango wa sehemu ya kukaushia ili kuzuia nzi.
Hakikisha kwamba unasafisha mikono kabla ya kugusa achari. Baada ya kila masaa 4, angalia kama vipande vimekauka vizuri kwa kuvibonyeza mkononi. Vipande vinapaswa kukaushwa hadi vigeuke manjano. Vipande vinapokauka kuwa hudhurungi hupunguza ubora. Fungasha vipande vya maembe ili kuzuia unyevu kuingia na kisha vihifadhi kwenye chumba kikavu kisicho na joto. Fungasha achari katika pakiti ndogo ukiwa tayari kuuza.