Kupogoa miti ya embe ni muhimu kwa njia kadhaa. Changamoto kubwa ni kujibu maswali kama vile; ni kipi kinapaswa kukatwa, wapi, lini na vipi.
Kimsingi, kupogoa huanza baada ya mti kupandwa na hii huitwa kupogoa kwa mafunzo. Wakati wa kupogoa, kata matawi yanayokua wima yaliyo katikati ili kuunda nafasi ya mzunguko wa hewa na jua kwenye matawi. Pia kata matawi yote ambayo hayasaidii mti kutoa matunda na acha tu matawi yanayotoa matuda. Baada ya kupogoa, ni muhimu kuondoa nyenzo zote zilizokatwa kutoka shambani mwako kwani zinaweza kuoza na hivyo kuvutia wadudu na magonjwa.
Mchakato wa kukata
Ni vyema kuanza kupogoa mti ukiwa ungali mchanga kwa sababu kadiri mti unavyokua bila kukatwa, ndivyo inavyokuwa ngumu kuukata.
Ili kupogoa mti mchanga wa embe, fanya mkato wa kwanza 60 cm hadi 80cm kutoka ardhini. Matawi 4 hadi 6 yatachipuka. Lakini chagua na uache tu matawi 3 hadi 4 kulingana na afya na nguvu ya mti, na pia pembe ambayo matawi yanaibukia. Matawi yanafaa kuwa yanakua katika pembetatu kamili au pembe mraba wakati yakiangaliwa kutoka juu.
Fanya mkato wa pili juu ya chipukizi. Matawi mengine 4 hadi 6 hutokea lakini pia acha tu matawi 3 hadi 4. Hakikisha kwamba hakuna matawi yanayokua katikati ya matawi mengine. Rudia kufanya utaratibu ulio hapo juu ili kukata mara ya mwisho.
Mara tu mti unapopogolewa awali, endelea kufanya upogoaji wa matunzo kila baada ya kuvuna ili kudumisha muundo mzuri wa mti.