Bakajani kahawia ni ugonjwa wa mpunga unaoenezwa kupitia mbegu, na husababisha mavuno duni ukishambulia mashamba na hivyo kusababisha kipato kidogo.
Ugonjwa huu huathiri mbegu, majani, mashina pamoja na nafaka hivyo kuugundua na kuudhibiti mapema ni muhimu. Bakajani kahawia ni ugonjwa wa ukungu ambao hubadilisha rangi ya majani na husababisha madoa ya kahawia. Bakajani kahawia kawaida husababishwa na mbinu duni za maandalizi ya ardhi.
Kuenea kwa ugonjwa
Ugonjwa wa bakajani kahawia huenea kupitia mbegu zilizoambukizwa, kwa hivyo inashauriwa sana kutumia mbegu zilizoidhinishwa. Kila wakati hakikisha unatibu mbegu kwa kuziloweka kwenye maji ya uvuguvugu au mchanganyiko wa viuakuvu kabla ya kupanda.
Udhibiti wa ugonjwa
Tayarisha ardhi vizuri kwa kuisawazisha ili kuzuia maji kutuama, na pia ondoa magugu ambayo yanashindana virutubisho vya mimea. Panda kwa kutumia mbegu zilizoidhinishwa kila msimu kutoka kwa wafanyabiashara wa kilimo walioidhinishwa. Ondoa magugu shambani ili kuzuia kuenea kwa magonjwa. Tumia mbolea bora za madini zilizosawaziswa baada ya kuchunguza na kupima rutuba ya udongo ili kuhakikisha ukuaji mzuri wa mazao. Mwagilia mashamba maji na kagua shamba mara kwa mara ili kutambua kwa urahisi mazao yaliyoathirika. Mwishowe, ondoa na uharibu mazao yaliyoathirika, na pia weka dawa za kuua ukungu zilizopendekezwa.