Viwavijeshi ni wadudu waharibifu wa mimea ya mahindi na husababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Hata hivyo, mbinu jumuishi za usimamizi hupunguza uvamizi wao.
Kukagua mahindi, kudhibiti viwavi mapema pamoja na kutumia viuatilifu visivyoharibu mazingira ni baadhi ya hatua bora zinazosababisha mavuno mengi na mapato ya ziada. Mabuu ni hatua ya uharibifu zaidi, hata hivyo usikague shamba baada ya kunyunyizia viuatilifu kwani vinaweza kuathiri afya yako. Epuka safu zilizo ukingoni mwa shamba iwapo unachagua maeneo ya uchunguzi.
Kukagua viwavijeshi
Tafuta uharibifu wa majani kama vile mashimo madogo, kinyesi cha viwavi, na mashimo kwenye gunzi la mahindi.
Kagua shamba ukifuata muundo wa herufi W, kwanzia mita 5 kutoka ukingoni mwa shamba. Fanya uchunguzi mapema wakati majani ya mahindi yanajifunua. Kagua kila mmoja ya maeneo 5 yaliyochaguliwa.
Katika kila mmoja ya maeneo haya 5, angalia kati ya mimea 10 hadi 20 kwa dalili za uharibifu wa viwavijeshi. Rekodi idadi ya mimea iliyoangaliwa na mimea iliyoharibiwa.
Wakati mimea inapojifunua majani ya kwanza, unafaa kurekodi miche iliyoharibiwa. Wakati mimea imejifunua majani yote, chunguza majani 2– 4 mapya kujitokeza.
Rekodi mimea iliyoharibiwa kwa kila mimea 10 – 20 katika kila eneo. Iwapo angalau mimea 4 kati ya mimea 10 imeharibiwa, shauriana na mtalamu wa kilimo kuona kama thamani ya zao itazidi gharama ya ulinzi.