Wakulima wengi hufuga idadi ndogo ya nguruwe kwa kuchinjwa, kwa kuzaa nguruwe wachanga au kwa kuuzwa katika soko za mijini. Nguruwe wengine hufungwa kwa kamba wakati wa mchana na kuachiliwa usiku.
Nguruwe wanaoachiliwa kuzurura hushambuliwa sana na magonjwa, vimelea, vijidudu na wakiwa wadogo, wanaweza kushambuliwa na mbwa au wanyama wa porini. Kwa hivyo, ikiwa unafuga nguruwe kibiashara ni bora kuwalinda bandani wakati wote.
Faida za banda
Unaweza kufuatilia nguruwe na kuangalia ni kiasi gani wamekula, na kuzuia mazao kuharibiwa. Banda huruhusu kuwapa maji na chakula kwa urahisi, kufuatilia ukuaji wao, kukusanya kinyesi chao na kuzuia magonjwa. Banda huwapa nguruwe kivuli ili wasichomwe na jua, na kudumisha hali ya joto ya nguruwe kwa kuwa hawasumbuliwi wala kufadhaika.
Ujenzi wa banda
Wakati wa kujenga banda la nguruwe hakikisha linapata jua asubuhi tu na alasiri ili kuepuka kuwa moto sana. Upande wa banda unapaswa kuwa wazi ili liweze kuruhusu nguruwe kufikia eneo la nje na kukapata mwangaza wa juani.
Banda linapaswa kugawanywa katika sehemu mbili; sehemu iliyofunikwa ambapo nguruwe hulala na kulishia, na eneo la nje ambapo chombo cha maji huwekwa, paomoja na mahali pa kutolea kinyesi na kukojoa.
Uchaguzi wa vifaa vya ujenzi
Banda la nguruwe linaweza kujengwa kwa mbao na vigingi vinne au zaidi ili kuliinua kutoka ardhini. Sakafu hutengenezwa na vibao vyembaba kwa muachano wa takribani 2cm ili kuruhusu mkojo na kinyesi kushuka chini na kukusanywa kwa urahisi. Kwa ujenzi wa chini, sakafu linapaswa kuwa la saruji na mteremko kwa usafishaji rahisi. Mfumo wa kuweka takataka ya mbao au maganda bandani unaweza kutumika badala ya saruji.
Vifaa vigumu kama matofali hutumiwa kujenga kuta za banda, ambazo zinapaswa kuwa na mapengo ya kuruhusu hewa kuingia na kupoesha nguruwe. Eneo kati ya ukuta na paa linapaswa kuwa wazi ili hewa iweze kupenya vizuri, pengo linapaswa kuwa angalau 1m juu. Mabati au majani ya miti yanaweza kutumika kama paa.
Ukubwa wa banda hutegemea idadi, aina na umri wa nguruwe. Msongamano mkubwa husisitiza wanyama, kwa hivyo hawatakua vizuri na watashambuliwa sana na magonjwa. Nguruwe jike anapaswa kutenganishwa na watoto wake, lakini nguruwe dume wazima pia hutenganishwa na dume wenzao.